UKIMYA MBINU MPYA SIMBA NA YANGA?
UKIMYA
MBINU MPYA SIMBA NA YANGA?!....
Ni nadra sana kuelekea mpambano wa watani wa jadi kukosa
shamra shamra , tambo , mbwembwe na kila aina ya vituko ili mradi kila mmoja
kujinasibu ni bingwa kuliko mwenzake.
Majigambo kwa viongozi hususani wasemaji wa timu pia
mashabiki yamepungua sana na ukimya umetawala kwa kambi zote . Kilichobaki ni
kalamu za waandishi na sauti za watangazaji kujaribu kuinadi derby hiyo.
Mara nyingi ratiba ya ligi inapotoka wengi huvutiwa zaidi
kutazama tarehe ya watani wa jadi kukutana na kuanza kutambiana. Tambo ambazo
huanzia kwenye kipindi cha usajili na mechi za awali. Lakini msimu huu joto la
watani wa jadi kwa majigambo na mbwembwe za kila aina zimepotea.
Msimu uliopita wa 2015-16 kidogo tambo zilikuwa kali
lakini zikizaa tawi jipya la watani hao wa jadi nje ya timu hizo kongwe zaidi
nchini . Wasemaji wa vilabu hivyo yaani Jerry Muro kwa Yanga SC na Haji Manara
kwa Simba SC waliibuka videdea kwa kusuguana zaidi kwa tambo za utani wa jadi
kuliko timu zenyewe. Utani uliozaa majina mapya ya watani hao wa jadi "
wamatopeni " ikiwa kejeli kwa Simba SC na " wakimataifa " kama
tambo kwa Yanga SC kwa ushiriki wake michezo ya CAF . Simba nao wakajibu kwa
jina la chura wakibeza hali ya mafuriko pale jangwani.
Kufungiwa kwa Jerry Muro ni chanzo cha ukimya huu ?
akihesabika kama muhamasishaji mkuu wa mashabiki wa Yanga SC kuipenda timu yao
na kuwananga Simba SC msimu uliopita ? Ukilitazama kwa undani suala hili
unaweza kuja na jibu la moja kwa moja kwamba ni kweli lakini kuna dhana
nyingine zaidi ya ukimya huu .
Mwamko kisoka kwa vilabu hivi viwili umeanza kuamka
hususani kwenye masuala ya kimsingi zaidi yaani kimbinu na kiufundi. Uwekezaji
katika masuala yasiyo na msingi yanaanza kutoweka na uwekezaji kwenye mambo ya
msingi kisoka yanashika hatamu . Uwekezaji kimbinu na kiufundi pia utawala bora
ndani ya timu na klabu kiujumla.
Kwa miaka mingi ilikuwa si muhimu sana kuiandaa timu
kimbinu na kiufundi kushinda mchezo huo lakini masuala ya kishirikina , rushwa
kwa waamuzi na hongo kwa wachezaji yakiaminika sana kuthaminiwa . Fedha nyingi
badala ya kutumika kuboresha mbinu na mipango ya ushindi kisoka , zilipelekwa
kwa mipango hiyo michafu kisoka .
Kila timu sasa inahitaji utulivu wa kambi yake kujijenga
kimbinu na kiufundi hali ambayo inawazuia viongozi , wachezaji na wanachama
wandamizi kuongea hovyo kabla ya mechi . Uimara wa timu zote unajenga pia hofu
kwa vilabu vyotr kujitapa kabla ya mchezo kwa kuogopa aibu ya baadae .
Historia za karibuni katika michezo ya watani hawa wa
jadi nayo inachangia kuua makali ya tambo za watani hawa jadi kabla ya mechi .
Unaweza kujitapa sana leo lakini baada ya mechi ukajikuta unachapwa na maneno
yako uliyoyatoa. Ushindi wa Simba SC 5-0 dhidi ya Young Africans May 6, 2012
linabaki jinamizi baya kwa viongozi , wanachama na wapenzi wa klabu hiyo hali
inayowanyima hali ya kujiamini mbele ya mashabiki wa Simba SC na vipngozi wao.
Vipigo mfululizo kwa Yanga SC kwenye kombe la mtani Jembe
pia ni kigezo kingine cha kuhifadhi maneno kwa mashabiki wa Yanga bahati mbaya
zaidi muda wote timu hiyo imefungwa ikiwa bora zaidi kimbinu na kiufundi dhidi
ya Simba SC .
Vipigo viwili mfululizo katika msimu wa ligi uliopita
ambavyo Simba SC ilivipata toka kwa Yanga SC ni jambo jingine linalochangia
kuzifunga pingu ndimi zao kujiachia kujitapa mbele ya Yanga SC . Bado
wanajiuliza vichwani mwao kuna uwezekano wa kupoteza mechi ya tatu mfululizo?
Pia usajili wa timu zote mbili msimu huu nao ni kigezo
kingine kinachochania kuleta hofu pande zote mbili kuliko kujenga hali ya
kujiamini kwa asilimia mia moja.
Ujio wa mfumaniaji mzuri wa nyavu Laudit Mavugo pale
Msimbazi akichagizwa na kasi za Ajibu na mwenzake Kichuya lazima inajenga hofu
kwa wapinzani hao endapo safu yao ya ulinzi ikiamka vibaya siku hiyo .
Achana na Chirwa ambaye bado hajawapa ngao ya kujitapa
mashabiki wa yanga kwa kushindwa kucheka na nyavu , Ngoma na mwenzake Tambwe
bado ni chem chem ya hofu kwa Simba SC . Tambwe akishirikiana na Busungu msimu
uliopita ndio walio waumiza hivyo bado wana hofu juu yao ingawa msimu haujawa
mzuri kwa Busungu lakini ujio wa Mahadhi bado ni hofu kwa Simba .
Mwisho ni mtazamo mpya wa waandishi na watangazi wanazi
wa timu hizi kuelekea mitanange hii ya watani wa jadi . Wengi sasa wanajikita
kutazama vitu vya msingi kisoka kuliko kuzipa kipaumbele tambo , kebehi na
nyodo za pande zote mbili kwenye redio na magazeti yao . Uchambuzi makini
kimbinu na kiufundi unawafanya mashabiki kupata hali halisi ya timu zao kabla
ya mechi hivyo kuwa na imani yenye mashaka kama turufu za wachambuzi zikiwapa
sababu ya hofu au kujigamba kiadi endapo ushindi unalalia kwao
Comments
Post a Comment