MKUMBUSHENI MANARA MPIRA SIO MCHEZO WA MALAIKA

Mkumbusheni Manara, mpira sio mchezo wa Malaika
Kalamu ya Ally Kamwe
ANAWEZA kuwa sawa kwa staili yake ya ufanyaji kazi. Kama viongozi wa Simba ambao ndio mabosi wake wanaridhishwa naye, mimi ni nani hadi niuponde utendaji wa Haji Manara?
Sina tatizo na kazi ya Manara pindi anaposimama na kuizungumza Simba. Tatizo langu linakuja pindi anapojaribu kuufanya mpira wa miguu uwe mchezo wa malaika.
Si sawa hili. Kama tukishindwa kumwambia sasa, tutapata shida sana kumweleza baadaye wakati akiwa ameshapata kundi la wafuasi wa kumwamini.
Haji anakosea sana kuchanganya mapungufu ya marefa kwenye maamuzi yao na hila za kuiumiza klabu yake. Hivi ni vitu viwili tofauti. Nitakwambia kwanini.
Tangu aingie madarakani, Rais wa Fifa, Gianni Infantino, amekuwa akifanya kazi kubwa ya kuingiza matumizi ya teknolojia kwenye soka kwa ajili ya kusaidia waamuzi.
Lakini mwisho wa siku changamoto zimekuwa nyingi kuliko faida. Kwanini? Sababu ni rahisi sana, soka ni mchezo wa binadamu.
Udhaifu wa kibinadamu ndio uliotengeneza ladha ya mchezo huu. Ndicho kitu kilichofanya kuwe na hisia mbalimbali za mashabiki katika kujadili baadhi ya mambo.
Mpira ni mchezo wa majibishano. Ni mchezo wa makosa. Kuanzia kwa wachezaji mpaka waamuzi. Ni kosa kutaka mwamuzi kuwa sawa kwa asilimia 100.
Nilimshangaa sana Haji Manara alipokuja na tv mbele ya waandishi wa habari na kuonyesha ‘clip’ za madai kuwa mwamuzi Elly Sassi aliwanyima penalti za wazi katika pambano lao dhidi ya Yanga.
Haijalishi hoja yake kama ilikuwa sahihi au la, ila msingi wa uwasilishaji wake ni wakitoto sana. hakutakiwa kufanya alichokifanya. Ni tukio la ajabu zaidi kufanywa na mtu mwenye uelewa wa mpira kama yeye.
Waamuzi ni binadamu. Makosa yao ya kibinadamu yanaweza kuinyima haki fulani Simba leo na kesho yakawanufaisha. Vipi atakuwa tayari kutoka hadharani na kudai kuwa ‘wamependelewa’?
Atakuwa na jibu gani siku timu fulani ikilalamika kuwa Simba walipewa bao la ‘offside’ au penalti isiyostahili? Atakuwa tayari kupindua matokeo akionyeshwa ‘clip’ za tv?
Juzi Arsenal waliumizwa na Manchester City kwa bao ambalo tv zote duniani zilionyesha kuwa ni ‘offside’, lakini mwisho wa siku, maamuzi ya refa yaliheshimiwa na maisha yameendelea.
Umewasikia Arsenal wakiitisha press na kuweka tv wakilalamikia tukio lile? Walichokifanya ni kusisitiza waamuzi kuongeza umakini kwenye maamuzi yao. Ilitosha sana.
Si wajinga Arsenal. Na si kwamba hawana tv majumbani kwao. Wanazo za kutosha lakini wametulia kwa sababu wanajua mpira wa miguu si mchezo wa malaika.
Makosa kama yale ni kitu cha kawaida sana kwenye mchezo wa mpira wa miguu.
Leo wameumia wao, lakini kesho huenda wakanufaika kwa makosa ya kawaida ya mwamuzi. Alichokifanya Manara ni kulitia aibu soka letu.
Kiongozi mkubwa kama yeye kusimama na kudai kuandika barua kwa Waziri kwa kosa la mwamuzi, ni kujikosea na kuukosea heshima mchezo wa mpira kwa ujumla.
Angeweza kulalamika na kuishia kupeleka malalamiko yake sehemu husika kwa mujibu wa kanuni zetu, si kuleta tv na kupeleka barua wizarani. Ili iweje sasa? Sidhani kama kuna haja ya kumkumbusha Haji mipaka yake ya kazi.
Tukiendelea kukaa kimya na kuona kama alichokifanya Manara ni kitu cha kawaida, Waziri Harrison Mwakyembe, atapokea barua ngapi ofisini mwake juu ya mapungufu ya waamuzi wetu?
Anachojaribu kutufundisha Haji Manara ni kulalamika katika kila kitu. Mpira wa miguu hauko hivyo.

Juzi alizitumia clip za Azam Tv kuwazodoa waamuzi, tusishangae siku akirudi tena kuwaponda Azam Tv, kwa kushindwa kuonyesha tukio fulani uwanjani. Tutampinga kwa lipi ikiwa hili tulikaa kimya?

Comments

Popular posts from this blog

Education for liberation and self-reliance By J.K.NYERERE

MABINGWA LIGI KUU TANZANIA TANGU KUANZISHWA KWA LIGI KUU 1965

MALALAMIKO MCC KUHUSU GOLI LA KICHUYA YATU BODI YA LIGI NA TFF