NI LWANDAMINA VS HANS VAN PLUIJM LEO

LWANDAMINA VS HANS VAN PLUIJM JUMAMOSI HII
Jumamosi hii wapenzi wa ligi kuu Tanzania bara wanakwenda kushuhudia moja ya mechi yenye gumzo la aina yake ambayo toka kuanza kwa ligi ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa .
Hii ni mechi kati ya mabingwa watetezi Yanga dhidi ya wageni wa ligi Singida United itakayopigwa katika dimba la Namfua mjini Singida baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa wa kupandwa nyasi upya sehemu ya kuchezea .
Hans Van Pluijm kocha mkuu wa Singida United kwa mara ya kwanza anakutana katika ligi kuu na timu ambayo kwa nyakati tofauti ameifundisha na kuipa mafanikio makubwa . Hans Van Pluijm mwenye falsafa ya soka la kidachi kushambulia muda wote , aliweza kuipa Yanga vikombe viwili vya ligi kuu Tanzania bara , Ngao ya jamii , Azam Sports Federation Cup na msimu wa 2016 kuwafikisha hatua ya makundi kombe la Shirikisho barani Afrika .
Huyu ndie aliyemwachia kijiti George Lwandamina ambaye anaionoa Yanga SC kwa sasa akiwa tayari ameendeleza wimbi la ushindi kwa kuwapa kombe moja la ligi kuu hali inayomfanya kusimama mbele ya mtangulizi wake jangwani kama bingwa mtetezi .
Tayari timu hizi zilikutana kwenye mechi ya kirafiki jijini Dar es salaam kabla ya kuanza kwa msimu huu mpya wa ligi kuu na Yanga kuibuka washindi kwa goli 3-2 . Jumamosi Singida kulipa kisasi ? Dakika tisini zitaamua .
Singida ni moja ya klabu ambayo imefanya usajili mzuri msimu huu ikiwa na mseto mzuri wa wachezaji wazawa na wageni toka nje . Wanashika nafasi ya 5 katika msimamo wa ligi kuu baada ya kucheza mechi 8, wakishinda mechi 3, sare 4 na kufungwa mechi 1 hali inayowafanya kujikusanyia alama 13 katika msimamo wa ligi kuu.
Yanga wanakutana na Singida katika raundi ya tisa ya ligi baada ya kucheza mechi 8 na kujikusanyia alama 16 kibindoni wakishika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu wakitanguliwa na mnyama Simba SC kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa . Yanga imeshinda mechi 4 na kwenda sare mara 4.
Pluijm anasifika kwa kuijenga vyema timu katika mfumo wa kujilinda . Ni mmoja wa waalimu ambao wana uwezo mkubwa kumsoma mpinzani wake na kujiandaa vyema dhidi yake aidha kujilinda au kujilinda na kushambulia kutafuta matokeo. Licha ya ugeni wa timu yake ligi kuu ambayo kwa sehemu kubwa inaundwa na wachezaji wapya , lakini mpaka sasa Singida imepoteza mechi moja tu kati ya nane ilizocheza kitu ambacho kitampa mtihani mkubwa Lwandamina kusaka ushindi dhidi yake nyumbani kwao.
Ni wakati mzuri kwa Lwandamina kuthibitisha ubora wake mbele ya mashabiki wa Yanga ambao bado wana ushabiki kindakindaki na mzee Hans Van Pluijm na tayari Lwandamina alianza kuonesha cheche zake katika mechi iliyopita dhidi ya Simba SC timu yake ikicheza vyema licha ya matokeo ya sare ya 1-1.
Tayari vijana wa Lwandamina wameanza kufunguka hivyo licha ya Hans Van kuijua vyema timu hiyo lakini huenda Lwandamina akaja na mbinu mpya na kushinda mchezo huo hususani eneo la kiungo ambalo kwa sasa linasimama kama roho ya timu hiyo chini ya viungo Tshishimbi na Ibrahim Ajibu. Mudathiri Yahya kiungo mkabaji wa Singida United sambamba na Tafazwa Kutinyu ambao mara nyingi hutengeneza pacha ya kiungo wana kazi ya ziada kuzima kasi ya muunganiko wa Tshishimbi, Ajibu na Rafael Daudi.
Dani Usengimana kwenye safu ya ushambuliaji ya Singida ni mchezaji wa kuchungwa na beki ya Yanga SC ambayo inakwenda kuwavaa Singida bila mlinzi wao mahiri Juma. Abdul mwenye kadi tatu za njano . Usengimana anaecheza kama false ten sambamba na Simbarashe , aliibuka mfungaji bora wa ligi ya Rwanda msimu uliopita hivyo analijua vyema lango.
Ni mechi ambayo ina mvuto wa aina yake ikilenga kupima uwezo wa waalimu wote hao wawili.
Na Samuel Samuel
USIKOSE MAKALA INAYOFUATA KUELEKEA MCHEZO HUO IKILENGA KUELEZEA TIMU ZOTE KIMBINU NA KIUFUNDI

Comments

Popular posts from this blog

Education for liberation and self-reliance By J.K.NYERERE

MABINGWA LIGI KUU TANZANIA TANGU KUANZISHWA KWA LIGI KUU 1965

MALALAMIKO MCC KUHUSU GOLI LA KICHUYA YATU BODI YA LIGI NA TFF