TATHIMINI YANGA ILIVYOCHEZA NA KMC

JINSI YANGA ILIVYOCHEZA DHIDI YA KMC
Usiku wa jumapili ya tarehe 8 Octoba 2017 katika uwanja wa Azam Complex kulikuwa na mechi ya kujipima nguvu kati ya mabingwa watetezi wa ligi kuu nchini Yanga SC dhidi ya timu ya ligi daraja la kwanza Kinondoni Municipal Council. Mechi hiyo imemalizika kwa sare tasa ya 0-0.
JUMLA
Mchezo kwa ujumla ulikuwa mzuri timu zote zikicheza kwa umakini mkubwa. Umakini katika kujilinda na kiasi katika kujenga mashambulizi lakini kwa ujumla wake timu zote zilifunguka na kuonesha uwezo halisi wa vikosi vyao katika mizani ya kimbinu na kiufundi. KMC hawakuogopa ukubwa wa Yanga muda wote walicheza kwa kujiamini na nidhamu kubwa kwenye mifumo yote ya kujilinda na kushambulia pia Yanga hawakuwadharau KMC kwa udogo wao kitu ambacho kiliufanya mchezo huu kuvutia zaidi licha ya kukosa magoli.
YANGA SC
Yanga SC wameingia uwanjani leo wakitumia mfumo wa 4-4-2 lakini kikosi chao kikiwa na sura nyingi mpya tofauti na wachezaji waliozoeleka kwenye mitanange ya ligi kuu nchini.
ULINZI
Safu ya ulinzi ya Yanga SC ilianza na Mwinyi Haji Kushoto na Hassani Kessy kulia kama walinzi wa pembeni huku Andrew Vicent na Festo Kayembe wakisimama kati. Mwinyi Haji ambaye toka msimu huu uanze hajapata nafasi yoyote ya kucheza katika mechi za ligi kuu, katika mchezo wa leo pia amedhihirisha kwanini Gadiel Michael aliyempora namba ni bora juu yake . Kwa kiasi alitimiza majukumu yake kama mlinzi lakini hakuwa msaada mzuri kwenye kusaidia kupandisha mashambulizi ya timu. Muda mwingi krosi zake pia pressing zilikuwa si nzuri . Hakuwa na muuanganiko mzuri na Mwashiuya kushoto kitu ambacho kiliwafanya KMC kutanua uwanja kwenye wing hiyo na mara nyingi mashambulizi ya kushitukiza yalipitia kwao. Gadiel ambaye hakuwepo katika kikosi cha leo kutokana na jana kuitumikia timu ya taifa , mara nyingi huwa aggressive kwenye nafasi hiyo kama wing back na krosi zake huwa na hesabu nzuri pia uwezo mzuri wa kukabia juu. Mwinyi anatakiwa kujitathimini sana kurudia kiwango chake cha misimu miwili iliyopita.
Kulia Kessy licha ya kukaa benchi muda mrefu , aliweza kucheza vizuri katika ulinzi na alipanda kusaidia mashambulizi ingawa na yeye kwa kiasi fulani pasi na krosi zake kwenye tatu ya mwisho ya kiwanja yaani eneo la ushambuliaji hazikuwa makini sana . Kutocheza mara kwa mara ni sababu lakini uzuri kwake aliweza kuwafinya KMC katika wing hiyo wakicheza vyema na Emanuel Martin aliyechezeshwa leo kama winga wa kulia.
Lwandamina aliamua kumpa nafasi mkongo Festo Kayembe ambaye amekuja kufanya majaribio kama mlinzi wa kati kwa ajili ya usajili wa dirisha dogo. Kayembe ambaye alikuwa akicheza kama mlinzi wa kati sambamba na Andrew Vicent, ameonesha uwezo mzuri sana . Amekuwa vyema kwa mipira ya juu pia kwenye one against one lakini bado hawakuwa na muunganiko mzuri na Vincent kwa sababu ni mara ya kwanza wanacheza . Muda mwingi walijikuta wanaingiliana kwenye maamuzi jambo ambalo kama KMC wangekuwa makini na kuwapa pressure kubwa basi huenda wangefanya makosa mengi na kutoa nafasi ya lango lao kushambuliwa . Kazi nzuri ya kiungo mkabaji Papy Tshishimbi alisimama kusahihisha makosa yao . Ni dhahiri Kayembe akicheza na commanding defender kama Kelvin Yondani basi Yanga wanaweza kuwa na ukuta imara sana . Licha ya kucheza kama mlinzi lakini pia ana uwezo mzuri Kayembe kuanzisha mashambulizi kutokana na foot work yake, pacing na uwezo wa kukokota mpira .
KIUNGO
Eneo la kiungo la Yanga leo lilikuwa vyema chini ya viungo wawili . Pappy Tshishimbi akicheza kama kiungo mkabaji ameendelea kudhihirisha uwezo wake. Alikuwa mwiba mkali kwa KMC katika kuvunja mipango yao ushambuliaji, kulinda walinzi wa kati pia kwenye kuipanga timu kwenye kushambulia pande zote ( tactical switching ) . Muunganiko wa Pappy na kiungo chipukizi Maka Edward ulikuwa mzuri na ndio walioweza kuwapoteza vijana wa Minziro pale kati . Maka akicheza juu alifanya kazi nzuri ya kusimamia mfumo wa kushambulia tatizo tu ni ubutu wa safu ya ushambuliaji ya timu yake ambayo leo ilikuwa inaongozwa Mateo Antony. Kazi nzuri ya Tshishimbi na Maka kwa njia ya kati ilikosa muunganiko mzuri kwa Yusufu Mhilu ambaye alipangwa kama kiungo mshambuliaji . Kupwaya kwa Mhilu kulimfanya Mateo kutopata mipira mizuri na mara nyingi akawa anacheza mbali na lango. Mhilu alikuwa akicheza sana chini na kuua umbo la ushambuliaji kitu ambacho kiliwapa kazi rahisi walinzi na viungo wa KMC kuwazuia .
Kwa kiasi kikubwa Yanga imekosa magoli kutokana na aina ya wachezaji ilyonao eneo la kati hususani viungo wa pembeni. Wengi wanamtumpia lawama Lwandamina lakini ukiangalia kwa umakini mkubwa wings za timu hii na washambuliaji wa kati ndio tatizo kubwa.
Toka msimu uanze uanze Mwashiuya hajawa na mchezo mzuri kuisaidia timu yake . Ana kasi nzuri kwenye pressing lakini anashindwa kuachia mpira kwa wakati na wakati mwingine anakaa sana na mpira kitu ambacho kinawapa wapinzani muda wa kujipanga . Si mzuri kwenye marking anapopoteza mpira hivyo kama angekuwa makini kwenye attacking patterns basi angeisaidia timu kujilinda kwa kushambulia . Msimu uliopita wing hii ilikuwa ikiwatupia Haruna Niyonzima na Deusi Kaseke . Haruna aliweza kujenga mashambulizi kwa maana ya pasi zake zenye macho huku Kaseke akiwa vyema kwenye marking pia kutoa krosi za uhakika pia kuingia kati kusaidia ulinzi. Hili ndio Lwandamina analikosa hivi sasa na ndio maana muda mwingi akimtumia kocha wake msaidizi Nsajigwa walikuwa wakimuelekeza Mwashiuya kucheza vyema .
Wing ya kulia bado ni mtihani mkubwa kwa Yanga toka kuondoka kwa Saimoni Msuva. Lwandamina amekuwa akijaribu sana kuisuka wing hiyo kurudisha makali yake ya msimu uliopita kwa kujaribu wachezaji mbalimbali. Alianza na Rafael Daudi lakini hakuweza kuimudu na kuamua kumrudisha kati. Juma Mahadhi ambaye wengi waliamini angeweza kuvivaa viatu vya Msuva lakini nae bado ni mtihani mkubwa kwake.
Mechi ya leo Lwandamina kamuanzisha Emanuel Martin kulia licha ya yeye kutumia mguu wa kushoto. Alichokuwa analenga mzambia huyo ni tactical overlapping ya Hassan Kessy na Martin. Alijua Kessy angekuwa anapanda juu na Martin kuvunjikia ndani kuongeza idadi ya washambuliaji mbele ya lango la KMC hivyo krosi za Kessy zingekuwa zinawakuta zaidi ya wachezaji sita eneo la ushambuliaji. Hilo lilikuwa la kwanza lakini pia kwa left footer anaepangwa kulia kama ana kasi ana uwezo wa kuisaidia timu kwenye kuing'oa timu pinzani kwenye muhimili wake wa ulinzi. Huwa wanakimbia juu kwa kasi kwenye wing ( dribbling ) kisha huingia kati ili kuutumia vyema mguu wao aidha kupiga langoni au kutoa pasi ya haraka ya mwisho ( switching to unlock ). Martin alijaribu kwa kiasi hili ingawa bado hakulitendea haki.
Kuingia kwa Buruani kulionesha kitu ndani yake ; uwezo wa kujenga mashambulizi na pressing kutokana dribbling yake ingawa anahitaji muda zaidi kujihakikishia namba kwa Lwandamina.
USHAMBULIAJI
Hili eneo bado ni tatizo kubwa kwa Yanga na mtihani mkubwa kwa Lwandamina. Wengi wana amini ujio wa Amisi Tambwe unaweza kulimaliza tatizo lakini binafsi naona kama benchi la ufundi la Yanga halitaweza kutengeneza viungo wazuri bado tatizo hili litaendelea . Viungo wazuri wa pembeni kuwalisha mipira mizuri watu wa kati ndio tiba kwa Yanga . Njia ya kati si tatizo kwa Yanga ; wana viungo wengi wazuri eneo hilo lakini si kama ilivyo kwenye wings .
Mateo amecheza mbali sana na mstari wa kushambulia kutokana na umbo la kushambulia la timu hiyo na tatizo lilianzia kwa viungo wa pembeni na pacha wake Mhilu. Mhilu mara nyingi alikuwa akicheza kama deep playmaker kitu ambacho Maka Edward alikigundua ndio maana alikuwa akipiga kutokea mbali hata alipoingia Juma Abdul kwa sababu wings zilishindwa pressing kwa maana ya kushambulia kwa kasi ili walinzi washindwe kutengeneza mtego wa kuotea . Timu ilikuwa flat.
Mwisho niseme licha ya kukaa nje kwa muda mrefu , Beno Kakolanya bado amerudi kwenye timu na kiwango kizuri kutoa ushindani chanya kwa mwenzake Youthe Rostand. Amewalinda vyema Yanga leo kutopoteza mbele ya KMC kwa kuokoa michomo mingi ya wazi.
Asanteni

Comments

Popular posts from this blog

Education for liberation and self-reliance By J.K.NYERERE

MABINGWA LIGI KUU TANZANIA TANGU KUANZISHWA KWA LIGI KUU 1965

MALALAMIKO MCC KUHUSU GOLI LA KICHUYA YATU BODI YA LIGI NA TFF