YANGA IMEKUWA NA JICHO LA MWEWE KWA SIMBA SC

YANGA IMEKUWA NA JICHO LA MWEWE KWA SIMBA SC
Anaandika mchambuzi Samuel Samuel
1997
Simba SC walishindwa kuzuia uhamisho wa Akida Makunda kwenda Yanga ambaye baadae aligeuka mwiba mkali kwa klabu hiyo na pia kusimama kama nguzo muhimu kwa Yanga safu ya kiungo na washambuliaji wa pembeni. Uhamisho wa kaka yangu huyu ni moja ya uhamisho unaosimama mpaka leo kama uhamisho wa uchungu sana kutokana na kiwango alichokuanacho Akida.
2007
Idd Athuman ' Chuji ' moja ya viungo bora kuwahi kucheza ligi kuu Tanzania bara . Alitua Simba SC mwaka 2006 akikutana na vijana wenzake wa miaka hiyo Henry Joseph , Kelvin Yondani na Victor Costa . Hakika walikuwa muhimili imara wa Simba SC kwenye kiungo na ulinzi bila kumsahau Ko'koo. Simba wakavurugana na Chuji . Kijana akafikia kusema ' kubaki Simba ni bora niuze ndimu ' . Yanga msimu wa 2007 wakamnyakua . Ubora wa Chuji Yanga na timu ya taifa ambao mpaka sasa hakuna aliyethubutu kuusogelea uliendelea kubakia jinamizi la mateso kwa wekundu wa msimbazi. Ikabaki kulaumiana tu . Ni mmoja wa wachezaji ambao walipikwa vyema na Maximo kusimama kama muhimili wa Taifa Stars eneo la kiungo cha chini. Goli lake dhidi ya Sudan mnalikumbuka?
2012
Kelvin Yondan ' Vidic ' ; wengi wanamwita mkandarasi . Huyu ni moja ya walinzi bora wa kati kwa zaidi ya misimu mitano sasa . Yondani aliondoka Simba kwa mizengwe tu mwaka 2012 na ameweka rekodi ya toka aondoke timu hiyo, Simba hawajafanikiwa tena kutwaa kombe la ligi kuu. Yondani ni aina ya wachezaji ambao wamekuwa na uwezo mkubwa wa kutunza vipaji vyao na kudumu katika ubora wao . Huyu bado anawasumbua mashabiki wa Simba ambao walimuhusudu vilivyo .
2013
Juma Kaseja moja ya walinda milango mahiri nchini, Novemba 8, 2013 kitita cha milioni 40 kilimuonesha njia mitaa ya Jangwani. Kaseja anatajwa kama mrithi wa mikoba ya Tanzania One ( halisi ) Mohamedi Mwameja . Nani anaweza kusahau kipaji cha Juma Kaseja akiwa kinda kabisa mwaka 2003 baada ya kuiwezesha Simba kuwang'oa mabingwa wa klabu bingwa Afrika msimu huo Zamaleki nchini mwao. Licha ya kutua Yanga bado alikuwa ni kipenzi cha wanamsimbazi. Masilahi yalimuondoa unyamani.
2014
Amisi Tambwe ' bataokota kunyavu'; Huyu aliitakatisha vilivyo Simba SC msimu wa 2012-13 akiibuka mfungaji bora wa ligi kwa magoli yake 19 lakini alijikuta akitupiwa virago na wekundu hao dakika za mwisho kabisa za usajili msimu wa 2014. Yanga waliamua kucheza kamari kwa kumsajili raia huyo wa Burundi ambaye baadae aligeuka mwiba mkali kwa Simba na timu kadhaa ligi kuu mpaka kuwafanya Simba kuanza kulaumiana kwa kumuacha. Tambwe bado yupo na Yanga ingawa kwa sasa ni majeruhi , ana mchango mkubwa na Yanga akiisaidia vyema kubeba ubingwa mara mbili mfululizo, kombe la ASFC na kuingia hatua ya makundi kombe la Shirikisho.
2016
Hassan Kessy ingawa bado hajawa na mafaniko ya kukumbukwa na Yanga kutokana na upinzani mkali wa namba na Juma Abdul kama walinzi wa pembeni kulia, bado Kessy ni zao bora toka Simba SC kutua Yanga . Ni mchezaji ambae kipaji halisi kinaonekana mguuni na kichwani kwa maana ya kutoa msaada au mchango wake pale anapohitajika. Mchezo wa jana dhidi ya Stand United alionesha nidhamu kubwa na ni moja ya mechi bora kwake tangu atoke Simba aliyocheza kwa utulivu na nidhamu kubwa . Lwandamina aliamua kumuanzisha Kessy kutokana na kadi za njano za Juma Abdul.
2017
Ibrahim Ajibu ; ni mapema sana kuhesabu mafaniko ya Ajibu na Yanga lakini ni mwendawazimu tu atabeza kipaji cha mshambuliaji huyo toka Simba kwenda Yanga. Katika mechi 7 amefunga goli 5 na kutengeza assists tatu kama sijakosea. Mwanzoni tu mwa msimu lakini tayari ameanza kuwafanya wanachama wandamizi wa klabu hiyo kukuna vichwa vyao.
Hawa ni baadhi tu wapo wengi kabla ya hawa..
SAMUEL SAMUEL

Comments

Popular posts from this blog

Education for liberation and self-reliance By J.K.NYERERE

MABINGWA LIGI KUU TANZANIA TANGU KUANZISHWA KWA LIGI KUU 1965

MALALAMIKO MCC KUHUSU GOLI LA KICHUYA YATU BODI YA LIGI NA TFF