''USALAMA WANGU UPO MASHAKANI''-NASARI
Siku tatu baada ya Mbunge wa Arumeru Mashariki,
Joshua Nassari (Chadema), kuibua tuhuma nzito dhidi ya viongozi wa serikali
waliowashawishi madiwani wa chama hicho kujizulu na kuhamia CCM, mbunge huyo
amesema maisha yake kwa sasa yako shakani.
“Usalama wangu kwa sasa upo shakani, watu wangu
wa karibu, familia yangu na wale wote nilioshirikiana nao kutekeleza jambo hili
wote hatuko salama,” alisema Nassari.
Mbunge huyo amesema hayo katika mahojiano maalum
na gazeti hili jijini Dar es Salaam yaliyolenga kujua chanzo na mikakati
aliyoitumia kufanikisha uchunguzi huo.
Jumapili iliyopita, Nassari na Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema (Chadema) waliweka hadharani sehemu ya video inayowaonesha
watu waliodai ni Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, mkurugenzi wa halmashauri hiyo na
katibu tawala wa wilaya jinsi walivyopanga na kufanikisha madiwani hao kujizulu
kisha kujiunga na CCM kwa lengo la kumuunga mkono Rais John Magufuli.
Katika mazungumzo yake, Nassari alisema:
“Nimebadili mfumo wa maisha, kwa sasa natumia usafiri ambao hauna hadhi kabisa
ya mbunge, kuna wakati napanda bodaboda, navaa miwani ili kujiziba watu
wasinitambue, natafutwa na kuna mmoja ameshanitumia ujumbe.”
“…hata kuja huku (Dar es Salaam kutoka Arusha)
nilitamani kupanda ndege lakini niliogopa, kwa kuwa kuanzia uwanja wa ndege
ningejulikana, kwani kuna watu wao hivyo niliamua kutumia njia ya barabara tena
kwa usafiri ambao huwezi kuamini anautumia mbunge na kama kungekuwa na usafiri
wa bajaji kutoka Arusha ningeutumia,” aliongeza:
Nassari alisema: “Hata hizi simu zangu kwa sasa
silali nazo najua wanaweza kuzifuatilia, jana nililala kwingine na simu
zilichukuliwa na Halima Mdee (Mbunge wa Kawe-Chadema) na Bulaya (Ester Bulaya-
Mbunge wa Bunda Mjini-Chadema).”
Alisema tangu suala hilo litokee, amekuwa akipokea
ujumbe na kupigiwa simu na watu wake wa karibu wanaonyesha wasiwasi juu ya
usalama wake.
“Kwa ushahidi huu, tumewavua nguo wateule na
waliowateua kwa hiyo si jambo dogo kiusalama, mkuu wa wilaya ndiye mwenyekiti
wa kamati ya ulinzi na usalama, anaweza kukufanya lolote kwa hiyo lazima
nichukue tahadhari,” alisema Nassari na kuongeza:
“Nilidhani Rais angekuwa tayari amewachukulia
hatua wote waliohusika ili kupisha uchunguzi unaofanywa na Takukuru (Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa), kwani uchunguzi hauwezi kufanyika kwa watu
ambao bado wako ofisini wanaweza kuuvuruga,” alisema
Nassari alisema ushihidi alioutoa Takukuru
ikibainika ni wa uongo atakuwa tayari kuachia ubunge wake na ikitokea
waliotuhumiwa wakaachwa atakuwa na wakati mgumu kuwatumikia wananchi wake wa
Arumeru Mashariki.
“Maisha yangu yatakuwa hatarini endapo watumishi
hawa wataendelea kuwepo ofisini ikizingatiwa kuwa ninapoishi na wanapoishi hao
sio mbali na hakuna mahali pengine nina makazi zaidi ya Meru,”alisema.
Ushahidi anaouzungumzia Nassari aliukabidhi juzi
Takukuru jijini Dar es Salaam na kuelezwa kwamba uchunguzi umekwisha kuanza.
Sabubu ya uchunguzi
Nassari alisema wakati akiwa masomoni nje ya
nchi, alianza kupata taarifa ya madiwani katika jimbo lake wanajiuzulu na wote
wakitoa sababu moja ya kwenda kumuunga mkono Rais Magufuli.
“Nilijiuliza nini kimetokea maana wote
waliojiuzulu wote walitoa sababu moja, watu wakasema mbona mbunge hasemi au
anahusika na yeye, mimi nikaamua kutafuta chanzo ili kupata ukweli na ndiyo
njia hii nilioyotumia,” alisema Nassari
Kuhusu vifaa na jinsi alivyovitega alisema:
“…siwezi kuweka mbinu hadharani, nilitumia mbinu za kijasusi, nikiweka wazi
nitakuwa naharibu, itoshe tu kusema ni vifaa bora kabisa vya kisasa ambavyo
vimefanikisha kupata ukweli na gharama ya vifaa hivi ni kama Sh 8 hadi 9
milioni.”
Alisema anashangaa mpaka sasa uchunguzi wa suala
la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) haujakamilika kwani
wakiruhusu wachunguzi wa kimataifa itafanikisha hilo.
“Unajua kwa teknolojia ya sasa, juu huko kuna
satellite ambazo ukiwaruhusu wachunguzi wa nje, watafunga mitambo yao katika
eneo hilo la Area D (mjini Dodoma) alipopigiwa Lissu risasi hizo na picha
zitaonyesha tukio zima,” alisema Nassari na kuongeza:
“Hata mimi naweza kuwasaidia kuwaunganisha na hao
wachunguzi, Serikali iruhusu wachunguzi wa nje ili kufanikisha hili na kupata
ukweli.”
Aligusia msimamo wa Serikali uliotolewa na Waziri
wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kwamba uchunguzi utafanywa na vyombo vya
ndani na wanasubiri Lissu apone aweze kusaidia.
“Nilitegemea Mwigulu asingekuwapo ofisini mpaka
sasa, anasema hadi Lissu apone, hivi kama Lissu angekufa uchunguzi
usingefanyika, hii ni kauli ya waziri wa mambo ya ndani ambayo sidhani kama
ilipaswa kuitoa,” alisema
By Ibrahim Yamola na Elizabeth
Edward, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz
Comments
Post a Comment