VITA YA WACHEZAJI YA YANGA NA SIMBA 28/10/2017 NI AJIBU AU OKWI?
KUTOKANA na viwango vya soka vilivyoonyeshwa na Yanga, Simba kwenye mechi
zao mwishoni mwa wiki iliyopita pamoja na takwimu walizokusanya baada ya mechi
saba za Ligi Kuu Tanzania Bara, inatoa picha halisi ya upinzani utakaokuwapo
kwenye mtanange wa watani hao wa jadi utakaopigwa Jumamosi hii.
Kwa sasa Simba ambao ni vinara wa Ligi Kuu Tanzania, wako moto na Yanga
wanaoshika nafasi ya pili pia ni moto, ambapo kwa watoto wa mjini wanasema ugali
moto na mboga moto.
Mpaka sasa mechi hiyo haijajulikana itachezwa wapi, ingawa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) limeonyesha kuwa mchezo huo unaweza kupigwa kwenye Uwanja wa
Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Lakini kutokana na mchezo huo wa Yanga na Simba kuwa ni moja ya ‘derby’ kubwa
barani Afrika, ukiziacha zile za Orlando Pirates na Kaizer Chiefs (Afrika
Kusini), Raja Casablanca vs Wydad Athletic Club (Morocco), Al Ahly vs Zamalek
(Misri), Club Africain vs Esperance Sportive de Tunis (Tunisia), bila shaka
Serikali inaweza kubadili maamuzi hayo na mchezo huo kuhamishiwa Uwanja wa
Taifa.
Pamoja na sintofahamu ya uwanja utakaotumika kwenye mechi hiyo, lakini
mtanange huo unatarajiwa kuwa wa kukata na shoka baada ya timu hizo kutoa dozi
kwenye mechi zao mwishoni mwa wiki iliyopita.
Ikiwa ni mara ya pili mahasimu hao kukutana msimu huu, baada ya ule mchezo wa
Ngao ya Jamii kwa ajili ya kufungua pazia la Ligi Kuu ambao ulimalizika kwa sare
ya 0-0 na Simba kubeba taji hilo kwa matuta 5-3.
Katika mchezo wa mwisho, Simba waliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya
Njombe Mji, kabla ya Yanga kujibu mapigo kwa kuichapa Stand United 4-0.
Matokeo hayo yamefanya timu hizo ambazo zimeshinda mechi nne na kutoka sare
tatu, kufikisha pointi 15 kila moja lakini Simba wakikaa kileleni kwa idadi
kubwa ya mabao ya kufunga, ambayo ni 19 wakati Yanga wakitingisha nyavu mara 10
pekee.
Mchezo huo utatoa picha ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na
upinzani uliopo, kwani atakayeshinda atakuwa atamwacha mwenzake kwa pengo la
pointi tatu, ingawa watakuwa na kazi kubwa kutokana na kufukuziwa kwa karibu na
Mtibwa Sugar ambayo pia ina pointi 15, huku kiwango chao msimu huu kikiwa
juu.
Ni mechi ya Ajib na Okwi
Kwa kiasi kikubwa mchezo utatawaliwa na majina ya washambuliaji Emmanuel Okwi
‘Mhenga’ wa Simba na Ibrahim Ajib (Yanga), ambao wameonekana kuwa moto wa kuotea
mbali kwenye upachikaji wa mabao msimu huu.
Okwi ambaye amerejea Simba msimu huu akitokea Sports Villa ya Uganda, tayari
ameshacheka na nyavu mara nane ikiwamo ‘hat-trick’ aliyopiga dhidi ya Ruvu
Shooting kwenye mchezo wao wa kwanza wa ligi walioshinda 7-0.
Naye Ajib ambaye alijiunga Yanga msimu huu akitokea Simba, ameshapachika
mabao matano, yakiwamo mabao yake mawili ya mpira wa adhabu ambayo yamekuwa
gumzo kwa mashabiki wa klabu hiyo ya Jangwani.
Pamoja na takwimu hizo za mabao kwa upande wa Okwi, lakini nyota huyo amekuwa
akifanya vizuri kwenye mechi hizo za watani wa jadi ambapo mabao yake mawili
aliyofunga wakati Wekundu wa Msimbazi wanaichapa Yanga 5-0 mwaka 2012, yamebakia
kumbukumbu kwenye vichwa vya mashabiki wa soka nchini.
Lakini hiyo imekuwa tofauti kwa Ajib ambaye alishindwa kutamba kabisa kwenye
mechi hizo akiwa Simba, ambapo kwenye mechi yake ya kwanza ambayo ilikuwa ni ya
Ngao ya Jamii, pamoja na kumaliza mchezo huo lakini hakuonyesha makali
yoyote.
Lakini mechi hii inawezekana ikawa tofauti kwa Ajib na akafanya maajabu na
kuibeba Yanga kutokana na kasi yake ya kupachika mabao, huku uzoefu wa Okwi na
kiwango anachoonyesha inaonyesha wazi kwamba mechi hiyo itakuwa ya aina yake
kwao na lolote linaweza kutokea.
Vita ya Tshishimbi na Mkude
Pamoja na safu ya washambuliaji ya timu hizo kupewa nafasi kubwa ya kung’ara
kwenye mechi hiyo, lakini utamu wa mchezo huo utakuwa kwenye safu ya kiungo
kutokana na kila mmoja kuwa na wachezaji imara.
Yanga wanamtegemea kiungo wao wa DR Congo, Papy Kabamba Tshishimbi, ambaye
tangu ametua msimu huu ameonyesha uwezo mkubwa na kukifanya kikosi hicho kuwa na
uhai kwenye safu ya kiungo.
Uwezo wa kiungo wa Simba, Jonas Mkude, unafahamika na mashabiki wa soka
nchini ingawa wawili hao hawatakutana moja kwa moja kutokana na kila mmoja
kucheza nafasi ya kiungo mkabaji, lakini wanaweza kukumbana kwenye eneo hilo na
kutakuwa na shughuli pevu.
Mashabiki wa soka nchini wamekwishaanza kujadili mchezo huo kwa upande huo wa
kiungo, kutokana na Mkude kurejea kwenye kikosi cha kwanza cha Simba baada ya
kuwekwa benchi mechi kadhaa, huku
Tshishimbi akiendelea kuwateka mashabiki wa Yanga tangu atue nchini akitokea
akitokea Mbambane Swallows ya Swaziland.
Hatima ya makocha
Mara kwa mara Yanga na Simba zinapokutana makocha ndio wanaoangushiwa jumba
bovu pale inapotokea timu mojawapo imepoteza mchezo huo wa watani wa jadi.
Kocha wa Cameroon anayekinoa kikosi cha Joseph Omog na mwenzake anayeinoa
Yanga, George Lwandamina wa Zambia, wote wanaonekana kukalia kuti kavu kutokana
na mwenendo wa vikosi vyao, ingawa bado timu ziko kwenye nafasi mbili za juu ila
mashabiki hao hawavutiwi na soka linaloonyeshwa.
Licha ya Omog kuisaidia Simba kurejea kwenye michuano ya kimataifa tangu
mwaka 2012, lakini amekuwa akionekana hana uwezo wa kukinoa kikosi hicho
kilichosheheni wachezaji nyota ambacho kilipaswa kishinde mechi zote ambazo
wametoka sare dhidi ya Azam FC, Mbao FC na Mtibwa Sugar.
Hali hiyo inayomkumba Omog inaendana na ile ya Lwandamina, ambaye anaonekana
hafai baada ya kutoka sare na Lipuli iliyopanda daraja msimu huu, kabla ya
kutoka sare nyingine na Majimaji kisha na Mtibwa.
Hivyo matokeo mabaya kwa upande wowote kwa timu hizo yanaweza yakasababisha
kocha mmojawapo kufungashiwa virago vyake.
Manula na Rostand
Mchuano mwingine utakuwa kwa makipa wa timu hizo, Youthe Rostand wa Yanga na
Aishi Manula ambao kwenye Ngao ya Jamii walipokutana Agosti 26, mwaka huu
hakuna aliyeruhusu bao.
Tangu msimu huu uanze, Rostand ameruhusu mabao mawili, huku Manula akiruhusu
manne na kuonyesha wazi mchezo huo utakuwa na upinzani mkubwa kila idara.
Comments
Post a Comment